Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Mstaafu Mary Longway (kushoto) akisaini kitabu cha wageni cha Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea baada ya kufika Ofisi ya Mkuu wa Shule hiyo Tupoke Ngwala (katikati).Kulia ni Mratibu wa Uchaguzi mkoa wa Ruvuma, Joel Mnemba.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea, Tupoke Ngwala (aliyevaa nguo ya kitenge) akitambulisha wageni kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa wanafunzi wa shule hiyo.Kulia ni Kamishna wa Tume hiyo Mhe. Jaji Mst. Mary Longway.
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Mst. Mary Longway akiwasalimia wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea baada ya kuwasili shuleni hapo kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura.
Ugeni kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi na meza kuu, ikiongoza wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea kuimba wimbo wa Taifa baada ya kufika ukumbi wa mikutano wa shuel hiyo kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea wakiimba wimbo wa shule hiyo.
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Mst. Mary Longway akitoa utangulizi wa elimu ya mpiga kura.Kushoto ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea, Tupoke Ngwala na kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria Bw. Emmanuel Kawishe.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria Bw. Emmanuel Kawishe akiwasilisha mada ya Elimu ya Mpiga Kura kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea. Kulia kwake ni Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Mst. Mary Longway na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea, Tupoke Ngwala.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea wakifuatilia elimu ya mpiga kura.
Baadhi ya walimu wa wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea wakifuatilia elimu ya mpiga kura.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea wakiuliza maswali baada ya kupata elimu ya mpiga kura.
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Mst. Mary Longway akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea Tupoke Ngwala, Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015, baada ya kuhitimisha elimu ya mpiga kura.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea Tupoke Ngwala akitoa neno la shukrani.
Picha na Hussein Makame, NEC
………………………………………………………………………
Hussein Makame, NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa Elimu ya mpiga Kura katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea mkoani Ruvuma na kueleza umuhimu wa elimu hiyo katika kuwawezesha wananchi na wadau wa uchaguzi kufahamu taratibu na hatua zote za uchaguzi hadi kutangazwa kwa matokeo.
Akitoa utangulizi wa elimu hiyo, Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mst. Mary Longway aliwataka walimu, wanafunzi na watumishi wa shule hiyo waliopata elimu hiyo wakawe mabalozi wa kuifikisha elimu ya mpiga kura kwa jamii inayowazunguka.
“Binafsi nategemea kila mmoja wenu ataweza kumuelimisha mwenzake ambaye hakupata nafasi kama hii ya kujua ni nini elimu ya mpiga kura” alisema Mhe. Jaji Mst. Longway.
Alisema Elimu ya mpiga kura ikitolewa humuwezesha mwanafunzi ambaye ni mpiga kura na mgombea mtarajiwa kufahamu sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura au mgombea.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume hiyo Bw. Emmanuel Kawishe alifafanua baadhi ya vipengele mbalimbali kuhusu uchaguzi ikiwemo kuweka utaratibu wa mtu kupiga kura kwenye kituo au eneo alilojiandikishia.
Alisema Kifungu cha 61 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinamruhusu mtu kupiga kura kwenye kituo alichojiandikisha na kwamba utaratibu huo huepuka baadhi ya sehemu kuwa na wapiga kura wengi kuzidi uwezo wakati vituo vingine vikikosa kabisa wapiga kura.
Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, Bw. Kawishe alizungumzia elimu ya mpiga kura kwa baadhi ya jamii zinazoishi maisha ya kuhamahama sehemu tofauti.
Alisema Tume inawajali wananchi wanaoishi kwa kuhamahama na inawafikia wananchi hao kupitia ushirikishwaji wa asasi za kiraia zinazokwenda kutoa elimu katika maeneo ya jamii hizo ili kuwafikia wananchi ambao ni ngumu kuwafikia.
“Wakati mwingine ili kuyafikia makundi hayo ya wananchi Tume inatumia ngoma na vikundi vya kiutamaduni kwenye maeneo husika, tunatumia redio za jamii za maeneo yale, kwa hiyo asipopata elimu kwa njia hii ataipata kupitia redio na njia za kitamaduni” alisema Bw. Kawishe.
Baadhi ya wanafunzi walizungumzia Elimu hiyo walisema wameridhishwa na Elimu waliyoipata na imewasaidia kufahamu mambo mengi yanayohusu Uchaguzi.
“Kwa kweli sisi wanafunzi wa Songea Girls tumefurahishwa sana kwa kupata elimu ya mpiga kura kwa kuwa imetusaiodia kujua haki zetu kama Watanzania hasa katika masuala ya uchaguzi” alisema mwanafunzi Faraja Samwel Sanga.
Kwa upande wake Husna Banda alisema amefurahi kupata elimu kuhusu kupiga kura na pia amejua umuhimu wa kupiga kura kumchagua kiongozi ambaye anampenda kwa ajili ya maedeleo ya taifa lake.
Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Shule hiyo Tupoke Ngwala alisema wanashukuru kwa nafasi ambayo wameipata ya kupata elimu ya mpiga kura na kwamba anaamini itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi na kuahidi kuifanyia kazi kwa kadri ya uwezo wao ili kufikia lengo lililokusudiwa.